WAZIRI MKUU AVUTIWA NA SHAMBA LA KAHAWA SONGEA
WAZIRI
MKUU Mizengo Pinda amesema amevutiwa sana na kazi iliyofanywa katika
muda mfupi kwenye shamba la kahawa la Aviv lililoko kwenye kijiji cha
Lipokela, wilaya ya Songea Vijijini mkoani Ruvuma.
Amesema
katika kipindi cha mwaka mmoja na miezi saba, eneo kubwa la shamba
limepandwa miche ya kahawa na mingine imezaa na imeshavunwa
ikilinganishwa na wakati alipofika shambani hapo Julai 2013 na
kutembelea tu kitalu cha miche ya zao hilo.
Ametoa
kauli hiyo jana jioni (Jumatatu, Februari 2, 2015) wakati akizungumza
na wafanyakazi na menejimenti ya shamba la Aviv baada ya kulitembelea na
kukagua miundombuinu ya umwagiliaji wa matone ya maji kwenye shamba
hilo.
“Mkuu
wa shamba hili, Bw. Medu amenieleza kwamba mpaka sasa, wameshavuna
kahawa mara moja na wanatarajia kuvuna tena hivi karibuni; lakini ili
waweze kuanza kupata faida ni lazima wavune mara nne.”
“Kilimo
kinataka uvumilivu na kinataka uwekezaji mkubwa... ni lazima kiwepo;
hata kwa wakulima wadogo ni lazima kiwepo licha ya ugumu wake. Sasa
ukisema kilimo ni kigumu na ukaacha kulima wakati una mke na watoto, je
hao watakula wapi?”, alihoji.
Aliwasifu
wamiliki wa shamba hilo kwa kuchagua kulima zao la kahawa kwani lina
walaji kila mahali ulimwenguni kote. “Wameamua kulima kahawa aina ya
Arabica ambayo inakubalika duniani. Uhitaji wa kahawa hii upo kila
mahali kwa sababu wanywaji wapo,” alisema.
Waziri
Mkuu alisema pamoja na mafanikio hayo, shamba la Aviv linakabiliwa na
changamoto ya nishati kwani linahitaji megawati 2.5 ili liweze kuendesha
mitambo yake ambayo kwa sasa inatumia mafuta yanayoligharimu fedha
nyingi.
Aliwataka wamiliki wa shamba hilo waendelee kuwa wavumilivu wakati Serikali ikiendelea kutafuta ufumbuzi wa suala hilo.
Mapema,
akisoma risala ya kampuni ya Aviv, Mkuu wa shamba hilo ambaye pia
anasimamia uzalishaji wa zao la kahawa Afrika Mashariki, Bw. Medu
Medappa alisema hadi sasa wamekwishalima hekta 1,060 na zote
zimekwishawekewa miundombinu ya umwagiliaji wa matone na kati ya hizo,
hekta 810 zimekwishapandwa miche ya kahawa.
“Shamba
letu lina ukubwa wa hekta 2,000 na hadi sasa tumeshalima hekta 1,060 na
zilizobakia ni kwa ajili ya kutunza mazingira na uoto wa asili kwenye
vilima vinavyotuzunguka,” alisema.
Alisema
hadi sasa wamekwishaajiri wafanyakazi 1,500 kwenye shamba hilo na kutoa
mafunzo kwa wakulima wanaoishi vijiji vya jirani. “Pia tumewapatia
miche ya bure kaya 673 na kutokana na mafunzo tunayowapa, wanavijiji
wameweza kulima kahawa inayoendana na viwango vya kimataifa vya
uzalishaji kahawa ambavyo ni miezi 22,” alisema.
Naye
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Bw. Said Mwambungu akijibu moja ya hoja kwenye
risala ya Bw. Medappa iliyohusu eneo la hekta tisa kuchukuliwa na Wakala
wa Ujenzi wa Barabara (TANROADS), alisema eneo hilo ni muhimu kwa
ujenzi wa barabara za mkoa huo kama ambavyo shamba hilo ni muhimu kwa
mkoa huo.
“Lile
eneo limetengwa na TANROADS kwa ajili ya kutengeneza kokoto za ujenzi wa
barabara. Barabara za lami tunazitaka. Tunahitaji kazi hii iendelee la
sivyo barabara zetu zitakufa,” alisema.
Alisema
watu wa TANROADS wakimaliza kazi yao, lile eneo litabaki tupu na
mwekezaji huyo anaweza kulitumia kadri atakavyoona inafaa kwa sababu
liko ndani ya eneo lake.
Post a Comment
HOME