LICHA YA CHANGAMOTO NYINGI BARA LA AFRIKA LINAPIGA HATUA - ZUMA
Na Ally Kondo, Addis Ababa
Wakuu
wa Nchi za Afrika wamekumbushwa kuwa, Mwaka 2015 umeingia lakini Bara
la Afrika bado linakabiliwa na changamoto nyingi ambazo kama
hazitapatiwa ufumbuzi ustawi wa bara hilo utaendelea kudumaa. Kauli hiyo
ilikuwa inarudiwa mara kwa mara na viongozi waliopata fursa ya
kuhutubia wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa
Umoja wa Afrika jijini Addis Ababa siku ya Ijumaa tarehe 30 Januari
2015.
Changamoto
hizo ni pamoja na mabadiliko ya tabianchi, ugaidi, migogoro ya kutumia
silaha, ukatili wa kutisha, biashara haramu ya binadamu, umasikini na
mlipuko wa ugonjwa wa Ebola. Walishauri katika mwaka wa 2015 lazima
matatizo hayo yajadiliwe kwa kina kwa madhumuni ya kuyatafutia ufumbuzi
wa kudumu.
Alipokuwa
anahutubia mkutano huo, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika,
Mhe. Nkosazana Zuma alisema kuwa, licha ya changamoto hizo, Bara la
Afrika linapiga hatua kimaendeleo na kwamba Agenda 2063 inayowasilishwa
katika Mkutano huo inatoa wito kwa Serikali na sekta nyingine
kushirikiana kwa pamoja ili kukuza uchumi kwa kuweka mkazo kwenye
ubunifu katika sekta ya kilimo, usindikaji wa mazao na ujenzi wa
miundombinu.
Mhe.
Zuma alisisitiza umuhimu wa kutumia fedha za ndani kwa ajili ya
kugharamia miradi ya kipaumbele ambayo imezingatiwa katika Mpango wa
Maendeleo wa Miaka 10 ambao nao utawasilishwa katika mkutano huo. Alieleza
kuwa Sekretarieti imefanyia kazi pendekezo la kutafuta vyanzo mbdala
vya fedha ambapo Mawaziri wa Fedha walijadili na ripoti yao
itawasilishwa wakati wa mkutano huo. Umoja wa Afrika pia umeanzisha
Mfuko Maalum utakaozinduliwa wakati wa mkutano huo kwa ajili ya
kuhifadhi fedha hizo.
Kwa
upande wake, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Mhe. Ban Ki-moon alieleza
kuwa mwaka 2014, AU na UN zilishirikiana kutafuta amani katika nchi
zenye migogoro. Alisema mafanikio makubwa yalipatikana na hivyo
kusisitiza kuwa pande zilizosaini mikataba ya amani lazima zitekeleze
vipengele vya mikataba hiyo. Alitoa mfano wa Mkataba wa Arusha na kusema
kuwa pande zinazohusika zitekeleze makubaliano ya kugawana madaraka.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa kukitokomeza kikundi cha waasi cha FDLR
kinachoendesha uasi wake Mashariki mwa DRC.
Mhe.
Ban Ki-moon pia aliwakemea viongozi wa Afrika wanaong’ang’ania
madaraka. Aliwashauri viongozi hao waache tabia hiyo na kuruhusu
demokrasia ichukue mkondo wake.
Rais
wa Kikao cha 69 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ambaye pia ni Waziri
wa Mambo ya Nje wa Uganda, Mhe. Sam Kutesa pamoja na mambo mengine,
alizungumzia mabadiliko ya mfumo katika Baraza la Usalama la Umoja wa
Mataifa. Alisema katika uongozi wake atafanya jitihada kuhakikisha kuwa
mfumo wa Baraza hilo, chombo ambacho alikitaja kama kisichokuwa na
demokrasia kuliko vyombo vyote duniani unafanyiwa mabadiliko.
Viongozi
hao pia walihimiza juhudi za kutafuta tiba na chanjo ya ugonjwa wa
Ebola na kusisitiza kuwa kampeni ifanywe ili nchi zilizoathirika na
ugonjwa huo zisamehewe madeni.
Post a Comment
HOME