0

MAKALA YA SHERIA: MNUNUZI WA GARI JIHADHARI NA UTAPELI HUU WA KIMKATABA

Na   Bashir  Yakub 

1. KUTAPELIWA  KATIKA  UNUNUZI  WA  GARI.

Ununuzi wa magari sawa na biashara nyingine yoyote unahitaji umakini. Lakini ununuzi wa  gari unahitaji umakini mkubwa zaidi pengine kuliko  mali nyingine yoyote inayohamishika kwa sasa. Hii ni kutokana na kukua kwa biashara ya bidhaa hiyo kulikoleteleza kujipenyeza  kwa matapeli hasa mijini. Utapeli  wa magari ni mkubwa kuliko watu wanavyofikiria na idadi ya wanaotapeliwa kwa siku inaelekea kulingana na idadi ya magari yanayouzwa kwa siku. Si  rahisi kulijua hili kama hufuatilii mambo haya. Uzuri au ubaya, wanaofanya matukio haya ni walewale. Nafasi kubwa wanayotumia ni ulaghai wa kimkataba na wanatumia mapungufu ya mkataba kumtapeli mtu halafu wanaendelea kuwapo na huna la kufanya sababu  mkataba wako una mapungufu ambayo uzito wake kisheria ni kama huna  mkataba. Aliyekutapeli atakuwapo na hutakuwa na la kufanya kwasababu ya msemo wa kisheria usemao “Buyer Be Aware”(Mnunuzi kuwa Makini). Umakini wako ni katika kufanya mkataba utakaolinda manunuzi yako. Lau ukifanya kosa  sheria imeshasema hivyo imemaliza. 

2. MKATABA SALAMA WA KUNUNULIA GARI  LAKO HAKIKISHA  UNA  TAARIFA   HIZI.

( a ) Lazima uwe na majina ya wahusika ambayo yatakuwa yameandikwa kwa urefu  na kwa kueleweka.Mfano jina liwe Aloys Mayenge Archard. Epuka kuandika vifupi  mfano A.M. Archard. Jina linatakiwa liwe katika ukamilifu wake na hasa pawe na majina matatu kamili. Pia majina  ya pande zote mbili yaani muuzaji na mnunuzi yatokee hivyohiyvo  si tu majina ya upande mmoja. Yawezekana mkataba mwingine unahusisha watu wengi zaidi  pia ni muhimu  majina matatu ya kila mmoja yaonekane hata kama  wako ishirini.

( b ) Katika majina hayo hadhi ya kila mmoja iainishwe mbele ya jina lake. Mfano kama ni muuzaji  au mnunuzi mbele iandikwe kuwa huyu ni muuzaji na huyu ni mnunuzi. Halikadhalika kama ni mkopaji, mkopeshwaji, mtoa zawadi mpokea zawadi viainishwe.

(  c  )  Bei au gharama halisi ya mauziano ioneshwe. Iandikwe kwa tarakimu yaani namba mfano 10,000,000/= na kwa maneno katika mabano ( Milioni kumi tu).Ni muhimu yote mawili yaonekane , hii huondoa utata.Tarehe ya mkataba ioneshwe sambamba  na maelezo kama fedha imelipwa yote au kiasi.

( d ) Kama kuna kiasi kilichobaki kianishwe kwa tarakimu na pia kwa maneno  kama nilivyoonesha hapo juu. Muda wa kulipa kilichobaki nao uainishwe ikiwa ni pamoja na hatua za kuchukua ikiwa muda uliowekwa utapita. Mkataba  lazima uoneshe muda ukipita  nini kifanyike mfano ikifika tarehe 7. 12. 2015 saa kumi jioni kiasi cha pesa iliyobaki hakijalipwa basi gari litamrudia muuzaji na mnunuzi hatakuwa na deni lolote dhidi ya muuzaji, au itahesabika kuwa mkataba umevunjika  na  mnunuzi atatakiwa kumlipa fidia ya kiasi fulani muuzaji kwa kuvunja mkataba.

( e  ) Mashahidi ni muhimu kila upande. Kila upande hata ukiwa na shahidi mmoja wala si mbaya. Shahidi awe mtu wa kuaminika , mtu mzima na mwenye akili timamu. Wataandika majina yao matatu kwa urefu kama yalivyo  ya wahusika  na pia wataweka sahihi zao huku  ikioneshwa shahidi yupi wa upande upi na yupi wa upande upi. 

(  f  ) Gari iliyouzwa au iliyohusishwa kwenye mkataba ichambuliwe vyema.Mfano chasis No, aina ya bodi,watengenezaji,rangi,namba kama imesajiliwa,uwezo wa injini,aina ya mafuta inayotumia,mwaka iliyotengenezwa n.k. 

( g )Mkataba  ni lazima ueleze gari imeingia nchini ikitokea wapi kama ni Japan,Dubai n.k.

( h ) Anuani za muuzaji au mnunuzi  ziwepo ikiwa ni pamoja na namba ya simu. Hili la namba ya simu  ni muhimu sana kwasasa kutokana na msaada mkubwa wa mawasiliano haya endapo mtu atahitajika.


( I ) Alama ya  dole gumba mbele ya jina nayo ni muhimu sana. Hii ni kutokama na alama hii kutoweza kwa namna yoyote kuingiliwa au kughushiwa.Tia dole kwenye kablasha ya muhuri na weka dole gumba mbele ya kila jina. Na hapa ndipo wanapokamatiwa matapeli walio wengi. Hatua hii pia si lazima kwa mashahidi.

( j ) Lazima mkataba ueleze kama gari imelipiwa leseni ya barabarani( road licence), bima, na kama ililipa ushuru wote muhimu unaotakiwa wakati wa kuingia nchini.Kama haijalipiwa baadhi au vyote mkataba ueleze na deni liainishwe. 

( k ) Ni muhimu pia  mkataba uoneshe iwapo gari lina tatizo lolote la kiufundi(machenical problem) kama hapana basi isemwe nini kifanyike kama muda mfupi baada ya manunuzi litagundulika tatizo ambalo muuzaji hakulisema. 

( L ) Pia ni muhimu sana mkataba uoneshe iwapo mgogoro wowote utatokea kuhusiana na mauzo ya gari nini wahusika wafanye, mfano endapo mgogoro utatokea kuhusiana na mkataba huu mahakama ya Tanzania yenye mamlaka  ndio itahusika na utatuzi wa mgogoro. Sambamba na hilo  mkataba uweke wajibu  kwa muuzaji kuwa tayari kumpa ushirikiano   mnunuzi iwapo  gari  alilomuuzia litakuwa na mgogoro kuhusu wizi,ushuru,mkopo, au mgogoro wowote unaotokana na mkataba wa mauziano hayo.

( M ) Aidha kipengele kinachomtaka muuzaji kurejesha fedha yote au sehemu yake iwapo jambo fulani litatokea pia chaweza kuwekwa.
3. TUSIPENDE  KUFANYA  MAMBO  KIENYEJI.
Muda wa kufanya mambo kienyeji umekwisha. Dunia imebadilika sana lazima watu walikubali hili. Ieleweke kuwa kufanya mambo kienyeji kuna gharama zake kubwa tu. Unaweza kuuziwa gari ambayo inatafutwa kwa kuua mtu jana. Unaweza kuuziwa gari ambayo inatafutwa kwa kushiriki katika  uhalifu mkubwa wiki iliyopita.Haya yote utayajibu vipi na yataisha lini. Unaweza kuuziwa gari ambayo haikulipa ushuru kwakuwa imesajiliwa kama inasafirishwa( IN TRANSIT,  IT) si ya hapa nchini, vipi utamaliza kesi na mzigo wa mamilioni ya deni la ushuru. Jihadhari ndugu epuka kufanya mambo kienyeji.
.
MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MSHAURI   WA  SHERIA  KUPITIA  GAZETI  LA  SERIKALI   LA   HABARI   LEO  KILA  JUMANNE  , GAZETI  JAMHURI   KILA  JUMANNE  NA  GAZETI  NIPASHE  KILA  JUMATANO.    
0784482959,        
 0714047241,         
bashiryakub@ymail.com

Post a Comment

HOME

 
Top