PAC yaishauri Serikali namna ya kuinusuru kampuni ya TTCL
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC),
Kabwe Zitto (kulia) na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Deo
Filikunjombe wakiwa katika majukumu yao. Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), Dk. Kamugisha Kazaura (kushoto) akiwa katika majukumu.
KAMATI ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imetoa mapendekezo ya
kuinusuru Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) kutokana na hali mbaya ya
kampuni hiyo kifedha kwa sasa ambapo inaendeshwa kwa hasara huku ikiwa
na madeni makubwa.
PAC
imetoa mapendekezo hayo katika taarifa yao kwa bunge ya mwaka juu ya
ukaguzi wa hesabu za Serikali kwa mashirika ya umma iliyotolewa Januari
28 mwaka 2015.
Kwa mujibu wa taarifa ya PAC hali ya mapato na matumizi ya TTCL kwa
mwaka 2012 ilipata hasara ya bilioni 20.883 huku kwa mwaka 2013 ikipata
hasara ya bilioni 16.258.
PAC
ilisema majumuisho ya hasara ya TTCL kupata hasara kwa takribani kwa
miaka 10, Kampuni sasa imekuwa na hasara ambayo kwa mwaka 2013 ilifikia
bilioni 334.48, jambo ambalo limeiondolea mvuto wa kukopeshwa na taasisi
za fedha hata zile zenye nia ya kuikopesha.
"...Ukosefu
wa fedha za kutosha kutekeleza miradi ya Kampuni umekuwa kikwazo kwa
TTCL kukabiliana na ushindani wa kibiashara. Kwa kipindi kirefu ufanisi
wa TTCL kiuwekezaji na kifedha umeendelea kudorora. Tangu TTCL
ibinafsishwe mwaka 2001, hakuna uwekezaji mkubwa uliofanyika na mpango
wa kutafuta mkopo kutoka mabenki ya ndani na nje ya nchi unakwamishwa na
masharti ya kupata udhamini wa Serikali," ilieleza taarifa hiyo ya
PAC.
PAC
iliongeza kuwa ukiacha madeni yaliopo pia TTCL inadaiwa na Mamlaka ya
Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA) jumla ya bilioni 25 hivyo
kufanya jumla ya deni kufikia bilioni 101.6. Kamati hiyo ya bunge
imesema kuna umuhimu wa Serikali kufanya maamuzi ya haraka ya kuikwamua
TTCL ili iweze kuendelea kutoa huduma kwenye Sekta ya Mawasiliano
ikizingatiwa kuwa ndiyo inayoendesha Mkongo wa Taifa wa mawasiliano.
Katika
mapendekezo ya PAC ili kuikwamua TTCL imeishauri Serikali kununua hisa
asilimia 35 zinazomilikiwa na Bharti Airtel katika TTCL kwa gharama
ndogo kwani Bharti Airtel haikutimiza kikamilifu masharti ya mkataba wa
mauziano ya hisa hizo hapo awali kwani tangu inunue hisa hizo haijafanya
uwekezaji katika Kampuni ya TTCL.
"...TTCL
isamehewe deni la Serikali Sh. 76.6 bilioni na deni la TCRA Sh. 25
bilioni ambayo jumla yake ni Sh. 101.6 bilioni na fedha hizo zipelekwe
kuongeza mtaji ili Kampuni itoke kwenye kuwa na mtaji hasi wa Sh. 87.896
bilioni na kuwa na mtaji chanya wa sh. 13.704 bilioni. Likifanyika hili
basi Kampuni hiyo itaweza kukopesheka.
Serikali
ikamilishe taratibu zake za kuimilikisha TTCL Mkongo wa Taifa ili izidi
kuuendeleza kwa ufanisi na kuongeza mapato ya TTCL," ilieleza sehemu ya
taarifa hiyo.
Hata hivyo PAC imeshauri kuwa kuna umuhimu wa kufanya marekebisho ya
muundo wa Kampuni ya TTCL kwani kwa sasa ina idadi kubwa ya wafanyakazi
(1549) isiyoweza kuwalipa.
Aidha,
ilibainisha kuwa kwa sasa zinahitajika bilioni 32 kwa ajili ya
kugharamia urekebishaji wa muundo wa Kampuni ili uendane na mahitaji ya
utoaji wa huduma mbalimbali.
Mashirika
mengine yenye hali mbaya kifedha na uendeshaji ni pamoja na Shirika la
Ndege Tanzania, ATCL ambayo kwa sasa ina madeni makubwa huku ikiwa na
ndege moja aina ya Dash 8–Q 300, Wafanyakazi 142 na Jengo la ATC House
lililoko mtaa wa Ohio, Dar es Salaam.
Post a Comment
HOME