Vijana jiwekeeni malengo kabla ya kukimbilia mikopo: Kongoye
Na: Genofeva Matemu - Maelezo
Vijana
kutoka Wilaya ya Mpwapwa na Kongwa Mkoa wa Dodoma wameshauriwa
kutokimbilia mikopo inayotolewa kwa vijana kabla ya kujipanga na kuwa na
malengo ya matumizi ya mikopo hiyo kwa maendeleo ya Taifa.
Rai
hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Bw. Christopher Ryoba
Kangoye wakati wa ziara ya maafisa kutoka Wizara ya Habari, Vijana,
Utamaduni na Michezo walipomtembelea ofisini kwake na baadae kukutana na
vijana wa wilaya hizo jana Wilaya ya Mpwapwa Mkoa wa Dodoma.
“Vijana
wamekua na tabia ya kukimbilia mikopo inayotolewa na taasisi mbalimbali
za serikali na zisizo za serikali kabla ya kujipanga hivyo kushindwa
kutumia fedha hizo kwa uangalifu na hatimaye kushindwa kurudisha mikopo
hiyo kwa wakati”, alisema Bw. Kangoye.
Aidha
Bw. Kangoye amesema kuwa vijana ni nguvu kazi ya taifa hivyo wanapaswa
kujitambua na kutumia nguvu hizo zitakazozalisha matunda mazuri kwani
ili mtu aweze kuendelea lazima afanye kazi kwa bidii na kwa ufanisi.
Akizungumza
kwa niaba ya maafisa kutoka Wizarani waliofika ofisini kwa Mkuu wa
Wilaya ya Mpwapwa Mwezeshaji kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni
na Michezo Bibi Ester Riwa amesema kuwa Wizara inayosimamia masuala ya
Vijana imepanga mikakati mingi ya kuwainua vijana wa taifa hili hivyo
kuiomba Wilaya ya Mpwapwa kushirikiana na Wizara inayosimamia vijana
kuwaongoza vijana wa Wilaya yao kuwa lulu ya taifa itakayomulika vijana
wengine kutoka Wilaya zote nchini Tanzania.
Kwa
upande wake Afisa Maendeleo ya Vijana kutoka Wilaya ya Mpwapwa Bw.
Paschal Jeremiah amesema kuwa vikundi vya vijana kutoka Wilaya ya
Mpwapwa vilipatiwa mkopo wa shilingi milioni 10 mnamo mwaka 2009 na
urejeshaji wa mkopo huo umefanyika kwa asilimia 90 hali inayoonyesha
kuwa vijana wa Wilaya yake wako makini na wanastahili kupatiwa mkopo
mwingine kuendeleza shughuli walizozianzisha.
Naye
kijana Briton Ivan Majele kutoka kikundi cha Umoja wa Vijana Ng’ambo
kilichopo Wilaya ya Mpwapwa kinachofanya kazi ya kufyatua matofali
amewataka vijana wenzake nchini kutobweteka bali wathubutu na kuamini
kuwa mtaji mdogo unaposimamiwa vizuri huzaa na kuwa mkubwa hivyo
kuthamini kile kidogo walichonacho na kukiendeleza.
Mkuu
wa Wilaya ya Mpwapwa Bw. Christopher Ryoba Kangoye akizungumza na ujumbe
kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo walipomtembelea
ofisini kwake kabla ya kukutana na vijana wa Wilaya ya Kongwa na Mpwapwa
kwa ajili ya kutoa elimu kuhusu Mfuko wa Maendeleo ya Vijana,
Ujasiriamali, Stadi za maisha na ujuzi jana katika Wilaya ya Mpwapwa
Mkoa Dodoma.
Mkuu
wa Kituo cha Vijana Sasanda Mbeya Bw. Laurean Masele akitoa mada ya
Uongozi kwa vijana wa Wilaya ya Kongwa na Mpwapwa wakati wa Semina ya
Ujasiriamali, Stadi za masiha, Ujuzi na Mfuko wa Maendeleo ya Vijana
iliyofanyika jana katika Wilaya ya Mpwapwa Mkoa wa Dodoma.
Vijana
kutoka Wilaya ya Mpwapwa na Kongwa wakifuatilia mada zilizokua
zikitolewa wakati wa Semina ya Ujasiriamali, Stadi za masiha, Ujuzi na
Mfuko wa Maendeleo ya Vijana iliyofanyika jana katika Wilaya ya Mpwapwa
Mkoa wa Dodoma.
Afisa
Maendeleo ya Vijana kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na
Michezo Bi. Amina Sanga akiangalia Cheti cha usajili wa Kikundi cha
Wapakaya kinafanya kazi ya kutengeneza Pikipiki kilichopo Wilaya ya
Mpwapwa walipowatembelea wanakikundi kwa ajili ya kukagua mradi wa
wanakikundi hao. Kushoto ni Afisa Maendeleo ya Vijana Wilaya ya Mpwapwa
Bw. Paschal Jeremiah.
Kijana
Ramadhani Khalid kutoka Kikundi cha Umoja wa Vijana Ng’ambo (UVING’A)
kilichopo Wilaya ya Mpwapwa kinachojishughulisha na ufyatuaji wa
matofali akishindilia mchanga katika mashine ya kufyatulia matofali
kuwaonyesha maafisa waliotembelea mradi wa kikundi hicho jinsi mashine
hiyo inavyofanya kazi. Kulia ni Mkuu wa Kituo cha Vijana Sasanda Mbeya
Bw. Laurean Masele na wapili kutoka kulia ni Afisa Vijana kutoka Wizara
ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Bi. Amina Sanga.
Afisa
Maendeleo ya Vijana kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na
Michezo Bi. Amina Sanga akishika jiko banifu linalotengenezwa kwa
kutumia udongo mfinyanzi kuangalia ubora wa jiko hilo lililotengenezwa
na wanakikundi cha Kujiamini kilichopo Wilaya ya Kongwa wakati wa
kukagua miradi ya Vijana wa Wilaya ya Kongwa Mkoa wa Dodoma.
(Picha zote na: Genofeva Matemu – Maelezo)
Post a Comment
HOME